FISADI NI WAHAINI….
Naanza changu kilio, Jamii sikilizeni,
Munitegee sikio, Na muketi vyema chini,
Dunia yaenda mbio, Yakaribia kingoni,
Fiasadi ni wahaini, Hukumu kali kupewa,
Leo niko uwanjani, Kutoa hisia zan
Kwa wote watanzani, Mlopatwa na machungu,
Wengi wetu masikini, Macho mekundu kwa kuni,
Fisadi ni wahaini, Hukumu kali kupewa,
Nchi imebarikiwa, Utajiri wa kufana,
Kusini kanda ya ziwa, Madini kila aina,
‘Tanzanite’ twaambiwa, Mfano wake hakuna,
Fisadi ni wahaini, Hukumu kali kupewa,
Kujiuzulu si shani, Hili tulitarajia,
Kwa vile vibilioni,Walojilimbikizia,
Hatuwa ilousoni, Mahakamani kungia,
Fisadi ni wahaini, Hukumu kali kupewa,
‘Senti’ walizonazo, Kutaifishwa wajibu,
Kwani huu ni uwozo, Hayo ndiyo matibabu,
Kwa wengine liwe funzo, Wasitamani jaribu,
Fisadi ni wahaini, Hukumu kali kupewa,
Serikali twaiomba, Imakinike na hili,
Yale mambo ya ujomba, Sasa iyatenge mbali,
Sasa iwe kama samba, Kuwan’gata mafedhuli,
Fisadi ni wahaini, Hukumu kali kupewa,
Muheshimiwa Raisi, Kumbuka ulotwambia,
Ari nguvu nayo kasi, Vyote ungevitumia,
Lakini tunavyohisi, Vyaanza kudidimia,
Fisadi ni wahaini, Hukumu kali kupewa.
Kassim Khamis Jape, (MUM), Morogoro, 0714694437 kjapes@yahoo.com
TUWAHESHIMU WAZAZI………..
Bismillahi naanza,Kwa jina la rahmani,
Naanza kwa kueleza,Kwa uwezo wa manani,
Ya faa kusikiliza,Kwa utulivu makini,
Tuwaheshimu wazazi, Tupate mafanikio.
Waze wawili tambuwa, Ndio ngao duniani,
Baba na mama elewa, Hawa ndio yako shani,
Ni vyema kuwakaguwa, Ikipitapo jioni,
Tuwaheshimu wazazi, Tupate mafanikio.
Ukutanapo wazazi, Kauli njema tumia,
Uwakatie mavazi, Wapate kufurahia,
Uwape mema matunzi, Chakula kuwapatia,
Tuwaheshimu wazazi, Tupate mafanikio.
Wazazi ni yako dira, Hilo yakini elewa,
Kaa nao kwa busara, Wasije wakachukiwa,
Utaipata hasara, Usiweze kujijuwa,
Tuwaheshimu wazazi, Tupate mafanikio.
Mama awali mwalimu, Ni yeye alokulea,
Alokufunza elimu, Hiyo unayoringia,
Sasa ni mtu muhimu, Jamii yakutambua,
Tuwaheshimu wazazi, Tupate mafanikio.
Wazazi wazazi wako, Ni kama mungu dunia,
Wasije wasije kwako, Na matusi watupia,
Watowapo kasiriko, Utakuja angamia,
Tuwaheshimu wazazi, Tupate mafanikio.
Wazazi watu muhimu, Qur-ani meshasema,
Ni budi kuwaheshuimu, Kwa kuwafanyia wema,
Usije kuwatuhumu, Utajutia daima,
Tuwaheshimu wazazi, Tupate mafanikio.
Kassim Khamis Jape, (MUM), Morogoro, 0714694437, kjapes@yahoo.com
0 comments on Kona ya Mashairi.
Add a comment
To add comments without entering your email and image verification, you must be logged in. Login or Join Blogster